Uongozi sio kazi (ajira) ni kuwatumikia wananchi

0
340

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika baadaye Oktoba mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema kuwa uongozi sio kazi (ajira) bali ni nafasi ya kuwatumikia wananchi.

Akizungumza katika kipindi cha Mizani kinachorushwa TBC kila Jumatano saa 3 usiku, Butiku amesema kuwa dhana ya uongozi sasa imepotoshwa, na watu wanachukulia kuwa kupata uongozi ni kupata ajira.

“Siku hizi imekuwa kutafuta uongozi ndio kitafuta kazi. Lakini kiongozi anapaswa kula wa mwisho. Uongozi ni mzigo, ukienda huko huendi kupata mali, bali unakwenda kufanya wengine wapate mali,” amesema Butiku.

Akizungumzia kauli ya Mwalimu Nyerere ambaye aliwashangaa watu waliokuwa wanakimbilia kuwa viongozi, Butiku amesema Mwalimu Nyerere alisema hayo kwa sababu uongozi ni mgumu, kwamba unapopita barabarani, kila unayemuona ni jukumu lako.

Amesema mara kadhaa Rais John Magufuli amekuwa akisikika akieleza namna uongozi ulivyo mgumu, na kwamba wakati mwingine analala kwa muda mfupi kwa sababu mambo yanayohitaji muda wake ni mengi, hivyo ukiona mtu anakimbilia uongozi hata kwa kuuza mali zake, huyo anapaswa kuogopwa.

Akizungumzia uhasama ambao huibuka wakati mwingine kutokana na siasa amesema, “Siasa si uadui, ni mazungumzo, lakini kuna kutofautiana. Kila kitu wote tukisema ‘ndiyo, ndiyo’ tutaonekana ni majuha.”