Umoja wa Mataifa waadhimisha miaka 74

0
247

Umoja wa Mataifa, leo unaadhimisha miaka 74 tangu ulipoanzishwa mwaka 1945.

Umoja wa Mataifa ulianzishwa ukiwa na Wanachama 51, na kwa sasa una Wanachama 193, huku Makao Makuu yake yakiwa huko Manhattan, New York nchini Marekani.

Kwa Tanzania maadhimisho hayo ya miaka 74 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa yamefanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kufanyika jijini humo.

Sherehe za maadhimisho hayo zimehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa waliopo hapa nchini pamoja na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

Mgeni Rasmi katika sherehe hizo alikua ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amezitaka nchi zote Wanachama wa Umoja wa Mataifa kudumisha amani na mshikamano.

Malengo makuu ya Umoja wa Mataifa ni pamoja na kulinda amani na usalama Kimataifa, kutetea na kulinda haki za binadamu, kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kulinda mazingira na kutoa msaada wa kibinadamu yanapotokea majanga ya asili, njaa na migogoro ya kivita.