Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akiongea na wajumbe wa Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) na Halmashauri zote za Mkoa (CHMT) na Wajumbe wa Timu ya Uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (RRHMT) wakati akihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Songwe.
“Naomba sana Mkuu wa Mkoa kupitia kwako kuwahimiza Wakurugenzi kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati ili wapate moyo wa kuendelea kutoa huduma katika vituo vyetu vya Afya,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Wakurugenzi wengine waige mfano wa Mkurugenzi wa Momba ambaye amewagawia viwanja watumishi wa Afya. Hivyo, lazima kuwajengea motisha na kuwavutia watumishi hao wa Afya ili waendelee kufanya kazi katika Halmashauri za Mikoa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, amemuomba Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kupeleka watumishi wa Afya hasa madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.