Ulega : Vituo atamizi fursa ya ajira kwa vijana

0
196

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha vituo atamizi vya kuwafundisha vijana ufugaji wa kisasa wa mifugo na samaki, lengo likiwa ni kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na waziri wa wizara hiyo Abdalah Ulega katika kongamano la tisa la wadau wa sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya sera.

“Kila mwaka zaidi ya vijana elfu moja wanahitimu ngazi mbalimbali za elimu kwenye vyuo vya mifugo ambapo kati hao 150 ndio hupata nafasi katika mfumo rasmi wa ajira , hivyo lengo letu ni kupunguza changamoto hiyo.” Amesema Ulega na kuongeza kuwa
“Katika mwaka wa fedha 2023/2024 mpango wetu ni kuwa na vituo atamizi 30 ambavyo vitakuwa na vijana wasiopungua 30 na kutufanya kuwa na vijana 900 ambao watakuwa wamepata mafunzo na hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji ajira nchini.”

Waziri Ulega ameongeza kuwa tayari wizara ya Mifugo na Uvuvi imeshatafuta masoko kwa ajili ya vijana hao kuuza mifugo yao, ambapo kwa mwaka watauza mifugo yao mara nne na hivyo kuwawezesha kupata kipato.