TAFIRI yatakiwa kufanya tafiti zenye tija kwa wavuvi

0
139

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetakiwa kujikita kwenye tafiti zenye tija kwa wavuvi wadogo na kushauri vyema kwenye mamlaka za serikali juu ya njia mbalimbali zikiwemo za kiteknolojia ili sekta ya uvuvi iwe na tija zadi kwa mvuvi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amebainisha hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo kujionea namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.

Akiwa katika ofisi za TAFIRI zilizopo Wilaya ya Kinondoni, Ulega amefafanua kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo ni lazima zijibu changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo hivyo ni muhimu kufikiria mambo ya kufanywa ili kuondoa changamoto hizo ikiwemo ya zana za uvuvi kutokana na mazingira ya sasa.

“Nyie ni wataalam wasomi lakini msiache kuwashirikisha na kuwasikiliza wavuvi ambao wamekuwa wakishinda baharini muda mrefu zaidi, mna mambo ya kujifunza kutoka kwao ili kuhakikisha mnawawekea mazingira bora ya kufanyia shughuli zao, ikiwemo kuhakikisha hawavui samaki kwa kuvizia bali wawe wanaelekezwa maeneo yenye samaki kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” amesema Ulega

Aidha, ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezeko la watu na mahitaji ya samaki, TAFIRI inapaswa kufikiria kwa kina zaidi kwa kufanya tafiti nyingi zaidi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI), namna ya kuhakikisha wananchi wa Tanzania hususani wadau wa sekta ya uvuvi wananufaika kupitia tafiti zenye matokeo chanya kwao.

Amesema ubunifu pekee ndiyo unaweza kuifanya TAFIRI kuwa karibu zaidi na wavuvi kwa kuwa watakuwa wanapata mafanikio kupitia uvuvi kwa tafiti ambazo zitawapatia zana sahihi za uvuvi kulingana na mazingira ya sasa pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kufahamu maeneo yenye samaki badala ya kuvua samaki kwa kuvizia maeneo ambayo hawana taarifa za uhakika juu ya uwepo wa samaki pamoja na majira yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dkt. Ishmael Kimirei amemuarifu Ulega kuwa taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha hali inayosababisha kushindwa kufikia baadhi ya malengo waliyojiwekea katika tafiti kutokana na ukosefu wa vifaa vikiwemo vya maabara.