Ukimya chanzo cha kuongezeka rushwa ya ngono

0
152

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimesema tatizo la rushwa ya ngono limekuwa kubwa lakini limeghubikwa na ukimya kutoka kwa walengwa, jambo linalosababisha tatizo hilo kuonekana kuwa sugu nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt Rose Reuben wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amewataka wananchi kupaza sauti ya kupinga rushwa ya ngono.

Amewataka waathirika kutoa taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua kukomesha vitendo hivyo.

Kwa upande Kaimu Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU mkoa wa Ilala, Elly Makala amesema suala la rushwa ya ngono limekuwa sugu katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo wao kama TAKUKURU wataendelea kufatilia matukio hayo ili wahusika watakaobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, ametoa wito kwa jamii kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vinajitokeza katika maeneo mbalimbali ya kazini, sokoni pamoja na viwandani.