Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, wabunge na waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto kufuatia kifo cha Askofu Getrude Rwakatare kilichotokea leo tarehe 20 Aprili, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na kifo cha Askofu Rwakatare ambaye amesema alikuwa mcha Mungu, mwenye upendo, asiye na majivuno, aliyepigania umoja na amani na aliyeipenda nchi yake kwa dhati.
Pamoja na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, Rais Magufuli amemuomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa wabunge wote na pia amewapa pole waumini wa kanisa hilo Askofu Rwakatare alikuwa kiongozi wake.
“Katika kipindi hiki cha majonzi, tumuombee Askofu Rwakatare apumzike mahali pema peponi, na nawasihi waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto muendelee kuwa wamoja na muendeleze mazuri yote yaliyofanywa na Mchungaji Rwakatare wakati wa uhai wake” amesema Rais Magufuli.
Raha ya milele umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Getrude Rwakatare astarehe kwa amani, Amina.