Ujerumani kuendelea kuisaidia JWTZ

0
612

Serikali ya Ujerumani kupitia mpango wa kusaidia Majeshi rafiki,  imekubali kuongeza kipindi cha kutoa misaada kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka minne zaidi kuanzia mwaka 2021hadi 2024 ambapo pamoja na mambo mengine itajenga hospitali kubwa ya kijeshi mkoani Dodoma.

Balozi wa Ujerumani nchini Dkt Detlef Wäechter akiwa na ujumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ametangaza uamuzi huo Ikulu jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Pamoja kujenga hospitali hiyo kubwa ya Kijeshi mkoani Dodoma,  Ujerumani pia imesema kuwa itaongeza mafunzo na vifaa vya ulinzi wa amani, itaendelea kufundisha madaktari wa Jeshi, kutoa vifaa vya matibabu na kutoa mafunzo ya ulinzi wa amani.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi ameishukuru Ujerumani kwa programu yao ya kusaidia katika sekta ya afya hapa nchini.

Mazungumzo hayo baina ya Balozi huyo wa Ujerumani nchini Dkt Wäechter na Rais Magufuli, pia yamehudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo na Katibu wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, – Malte Loknitz aliyeongoza ujumbe wa maafisa kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.