Serikali imepokea kivuko kipya cha MV CHATO II HAPA KAZI TU, ambacho ujenzi wake umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1.
Kivuko hicho kimejengwa na kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine ya jijini Mwanza, na kitakuwa kikitoa huduma kati ya Chato, Muharamba na Nkome mkoani Geita.
Akizungumza mkoani Geita wakati wa sherehe fupi ya kupokea kivuko hicho katika eneo la maegesho ya kivuko, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt Leonard Chamuriho amewapongeza Watendaji wa wizara hiyo pamoja na wale wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kusimamia vema ujenzi wa kivuko hicho hadi kukamilika kwake.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha usalama na usimamizi wa vivuko vyote nchini, ili kuepusha matukio ya ajali kwa kuwaweka maafisa kutoka TASAC kusimamia maeneo yote yenye usafiri wa majini na kuendelea kutoa mafunzo kwa waendesha vyombo hivyo.
‘’Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya Wananchi kwa kuendelea kuvifanyia matengenezo ya uhakika na kununua vipya pale vinapohitajika kadiri ya uwezo wa bajeti ya serikali unavyoruhusu,’’ amesema Dkt Chamuriho.
Kivuko cha MV CHATO II HAPA KAZI TU kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari madogo 10 sawa na tani 100 kwa mara moja, na kinafanya idadi ya vivuko hadi sasa kufikia 32 kote nchini.