Ujenzi wa meli MV Mbeya II wafikia asilimia 80

0
2196

Ujenzi wa meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II inayotarajiwa kutatua changamoto za usafiri wa abiria pamoja na mizigo katika mwambao wa ziwa Nyasa umefikia asilimia 80.

Meneja wa bandari katika ziwa Nyasa,- Abed Gallus amesema kuwa meli hiyo itakayokua ya kwanza ya kisasa ya abiria itaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Njombe na Ruvuma pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia.

Gallus amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo unaofanywa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine ni moja ya juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) katika kuboresha shughuli za usafirishaji wa abiria pamoja na mizigo majini.

“Ujenzi wa meli hii ya abiria, ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa meli tatu za TPA katika ziwa Nyasa zinazolenga kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo majini,” amesema Gallus.

Ameongeza kuwa,  TPA ilianzisha mradi wa meli tatu zikiwemo mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani elfu moja na moja ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200.

Ujenzi wa meli hiyo ya abiria ya MV Mbeya II unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni tisa.

Meli hiyo mpya ya MV Mbeya II inatarajia kufanya safari zake katika bandari mbalimbali kongwe na nyingine mpya zitakazoanzishwa na TPA katika mwambao wa ziwa Nyasa, lengo likiwa ni kuleta ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo.