Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameweka jiwe la msingi na kuzindua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Imalilo kilichopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Akizungumza wakati wa akiweka jiwe hilo la msingi,
Dkt Kalemani amesema kuwa Ujenzi wa kituo hicho utakamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa.
Ujenzi wa kituo hicho unatekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya shilingi bilioni 75 ambazo ni fedha za ndani.
Kuhusu Wananchi waliotoa maeneo yao kupisha ujenzi wa kituo hicho, Dkt Kalemani amesema kuwa tayari Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 47 kwa ajili ya kuwalipa fidia.
Ujenzi wa Kituo hicho cha kupoza umeme cha Imalilo kilichopo wilayani Bariadi utakapokamilika, kituo kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati mia moja za umeme zitakazotumika ndani ya mkoa wa Simiyu na mikoa jirani.
“Umeme utakaozalishwa hapa ni mkubwa utauwezesha mkoa huu na mikoa jirani kuendesha shughuli za viwandani na uwekezaji wa aina yoyote unaohitaji umeme mwingi”, amesema Dkt Kalemani.