Ujenzi wa Bwawa la Nyerere wafikia asilima 56

0
174

Waziri wa Nishati, January Makamba ameeleza kuwa, utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa bwawa la kuzalishia Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2115, kwa sasa umefikia asilimia 56 na kwamba Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kasi, uadilifu, ubora na viwango vinavyotakiwa ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Makamba ameeleza kuwa, mradi huo kwa sasa unatekelezwa kwa kasi kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika usimamizi na uendeshaji wa mradi huo ambapo alitaja baadhi ya maboresho hayo kuwa ni kuongeza utaalam na wataalam pia Mkandarasi wa mradi huo, ambaye ni kampuni ya Elsewedy Electric amehimizwa kuongeza wataalam wenye uzoefu wa usimamizi wa miradi mikubwa kama wa JNHPP.

Ametaja maboresho mengine kuwa ni mabadiliko ya uongozi katika mradi, kubadili mfumo wa mawasiliano kati ya Wizara na TANESCO pamoja na TANESCO na Mkandarasi pamoja na mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya TANESCO ambayo yamekuja na mbinu za kisayansi za kutekeleza mradi huo na matunda yake yameanza kuonekana.

Ameongeza kuwa, kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita mradi ulikuwa chini ya asilimia 40 lakini sasa umefikia asilimia 56 na kwamba malipo kwa Mkandarasi, kwa mwaka jana yaliyofanyika yalikuwa takriban shilingi Trilioni Mbili na kufanya malipo jumla kuaa shilingi Trilioni 3.4 tangu kuanza kwa mradi huo.