Ujenzi wa barabara ya juu eneo la Tazara wafikia asilimia 98

0
2278

Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere eneo la Tazara jijini Dar es salaam kwa asilimia 98.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa mwisho wa baraara hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo ya juu imefikia mahali pazuri na serikali inaendelea kuimarisha na kukamilisha miradi mikubwa nchini kama sehemu ya kutekeleza ahadi za serikali kwa Watanzania.

Amesema kuwa katika ujenzi huo ni vitu vidogo tu ambavyo bado havijakamilika ili kuwezesha watanzania kuanza kufaidi matunda ya serikali yao, jambo ambalo ni la kujivunia.

Ujenzi wa barabara hiyo unaofadhiliwa na serikali ya Japan umefikia asilimia 98, ambapo barabara na njia zote zimekamilika, taa pamoja na miundombinu mingine iko tayari na kilichobaki ni ujenzi wa kiwango cha juu pembeni mwa barabara hizo ili kuzuia udongo na mchanga kuingia katika barabara.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, ujenzi huo wa barabara ya juu katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere eneo la Tazara utarahisisha maisha ya wakazi wa Dar es salaam hasa wanaotoka maeneo ya Gongo la Mboto, Mbagala na Pugu kwenda katikati ya jiji kwa kuepusha adha ya foleni eneo la Tazara, pia abiria kutoka uwanja wa ndege kwenda katikati ya jiji watarahisishiwa usafiri kutokana na kupungua kwa foleni.

Waziri Mkuu pia ametembelea eneo la Ubungo ambako alikagua ujenzi wa mradi mkubwa wa barabara kuu ya Dar es salaam- Morogoro.

Akieleza mpango wa serikali wa kukamilisha ahadi zake kwa wananchi Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa serikali imejipanga kuwa mpaka kufikia Juni 2020 mradi wa Ubungo utakuwa umekamilika.

Amemuagiza mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, -Paul Makonda kutenga eneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga walioko Ubungo ambako ujenzi unaendelea ili wasiathiri utekelezaji wa mradi huo.