Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuongeza fursa za uwekezaji kwa wakulima na wafanyabiashara wa ndani na nje kusafirisha bidhaa zao na kuongeza pato la Taifa.
Waziri Mbarawa amesena hayo hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya mradi wa ujenzi wa barabara za maingiliano katika daraja la Sibiti, Noranga – Doroto na Itigi – Mkiwa katika halmashauri ya wilaya ya Itigi mkoani Singida.
Akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Mbarawa amesema hapo awali barabara hiyo ilikuwa ikitumika miaka ya 1970 kabla ya barabara ya TANZAM haijajengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha Profesa Mbarawa ameongeza kuwa, abiria waliokuwa wakisafiri kwenda Mbeya, Iringa na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini kutoka Kanda ya Ziwa walikuwa wakisafiri na treni hadi Itigi na kuchukuliwa na mabasi kwenda Mbeya na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila amesema, ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kuunganisha Ushoroba wa Tanzania na Zambia (TANZAM Highway Corridor) na ushoroba wa kati (Central Corridor) eneo la Mkiwa katika barabara ya Dodoma – Singida.