Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Elias Kwandikwa amezindua awamu ya Pili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Morogoro – Makutopora na kumtaka Mkandarasi kampuni ya Yapi Markezi ya nchini Uturuki kumaliza kazi hiyo kwa wakati.
Akizungumza wakati wa zoezi la utandikaji mataluma ya reli hiyo katika eneo la Kilosa mkoani Morogoro, Naibu Waziri Kwandikwa amesema kuwa, pamoja na kasi kubwa ya ujenzi wa Reli hiyo, Mkandarasi huyo anapaswa kumaliza kazi zote kwa wakati.
Naibu Waziri Kwandikwa amesema kuwa, ujenzi wa Reli ya kisasa unaofanywa na Serikali una lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za usafiri wa reli hapa nchini na nchi jirani.
Awali akitoa taarifa ya Ujenzi wa Reli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa amesema kuwa, asilimia 90 ya eneo linalohitajika kwa ajili ya ujenzi wa Reli hiyo kipande cha Morogoro – Makutopora limekabidhiwa kwa Mkandarasi kampuni ya Yapi Markezi.
Pamoja na kuzindua Ujenzi huo, Naibu Waziri Kwandikwa pia amepata fursa ya kutembelea eneo linapojengwa handaki refu zaidi kwenye ujenzi huo, lenye urefu wa Kilomita 1.4.
Awamu ya Pili ya ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) kipande cha Morogoro – Makutopora, Kina urefu wa zaidi ya Kilomita 400 na tayari Serikali imelipa Shilingi Trilioni 4.7 kwa ajili ya kutelekeleza ujenzi huo.