Ujenzi daraja la JPM wafikia 70%

0
124

Ujenzi wa daraja la J.P Magufuli linalounganisha eneo la Kigongo wilayani Misungwi na eneo la Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza umefikia asilimia 70, huku ujenzi huo ukitarajiwa kukamilika mwezi Februari mwaka 2024.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Boniface Mkumbo ametoa tathmini hiyo wakati akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani na ujenzi wa daraja hilo.

Mhandisi Mkumbo amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia ujenzi huo umeongezeka kutoka asilimia 30 hadi asilimia 70, ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 348 zimelipwa kwa mkandarasi na shilingi Bilioni 4.6 zimelipwa kwa Mhandisi Mshauri wa mradi huo.

Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi Bilioni 3.146 zimelipwa kama fidia kwa watu na mali zilizoathiriwa na mradi huo.

Kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda unaopotea kwa wananchi wanaotumia vivuko kwenda katika mikoa ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ambapo daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 litawawezesha kuvuka kwa kutumia dakika 4 badala ya saa nzima wanayotumia hivi sasa.