Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa chachu ya kushirikiana katika majukwaa ya kimataifa hususan kupambana na ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa umekithiri.
Kadhalika amesema Serikali zote zinatambua ni umoja pekee utakaowezesha kuvuka vizingiti na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo.
Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa Agosti 16,2019 katika Chuo cha Solomon Mahlangu kilichopo Mazimbu Morogoro nchini Tanzania wakati wa ziara ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Amesema nchi hizo zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria ambao umechagizwa na eneo la Mazimbu ambalo lilitumika kama kituo cha wapigania uhuru wa Afrika Kusini kujifunza namna ya kupambana.
“Mazimbu ni eneo lenye historia na linaonyesha uhusiano wa kihistoria baina ya nchi zetu mbili. Huwezi kuelezea uhusiano wa kihistoria kati ya Afrika Kusini na Tanzania bila kuitaja Mazimbu.”
“Tunapoongelea kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi Afrika Kusini daima tutawakumbuka Mwalimu Nyerere na Mzee Mandela kwa sababu ya utumishi wao wa kujenga misingi imara ya umoja na mapambano dhidi ya ubaguzi,” amesema Majaliwa