Uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Saudi Arabia kuimarika

0
145

Waziri wa Nishati, January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Abdulaziz bin Salman Al Saud kwa lengo la kuanzisha uhusiano kibiashara na kubadilishana ujuzi baina ya nchi hizi mbili.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Makamba amesema ameenda nchini Saudi Arabia akiwa na ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa ujumbe huo umefika kama ulivyokusudiwa.

Aidha, Makamba ameongeza kuwa Tanzania na Saudi Arabia zina mahusiano mazuri ya muda mrefu na sasa nchi hizi mbili zinakusudia kuendeleza mahusiano kwa kuongeza ushirikiano katika sekta ya nishati.  
 
“Katika kuthibitisha hilo siku za hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia alitembelea Tanzania na pia Mfalme wa Saudi, Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud amemualika Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kuzuru Saudi Arabia” ameeleza Waziri Makamba.
 
Waziri Makamba, katika ziara hiyo ameambatana na Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, ambapo Ziara hiyo imelenga kuanzisha uhusiano wa kibiashara, kubadilishana ujuzi na teknolojia katika sekta ya mafuta na gesi.

Ikumbukwe kuwa Saudi Arabia ni mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani na hivyo mahusiano na Tanzania yanaweza kufungua fursa mbalimbali katika eneo hilo.

Leo ni siku ya pili ya ziara ya kikazi ya Waziri Makamba nchini Saudi Arabia