Uganda watembelea Mradi wa Gesi asilia Kinyerezi

0
205

Ujumbe kutoka nchini Uganda umeipongeza Serikali ya Tanzania na kufurahishwa na utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi Mkoani Dar es salaam, baada ya kutembelea mradi huo.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba wakati wa ziara ya Ujumbe kutoka nchini Uganda uliohusisha Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini nchini Uganda, Dkt. Peter Lokeris na Kamati ya Bunge ya Mazingira na Maliasili nchini humo walipotembelea Mradi wa Kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezij Julai 21,2022.

Ujumbe wa Uganda uko nchini kwa ziara ya siku sita kwa lengo la kujifunza na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya Nishati,kuanzia Julai 19 hadi 24, 2022 katika Mkoa wa Dar es salaam na Tanga.

Mhandisi Mramba amesema kuwa wageni hao wameona na kufurahishwa na kazi kubwa ya uwekezaji iliyofanyika katika kutekeleza Mradi wa Kinyerezi, na kwamba wameipongeza serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi huo adhimu kwa nchi za Afrika Mashariki.

Amesema ujio wao ni uthibitisho tosha kuwa nchi hizo mbili sasa ziko tayari kushirikiana katika rasilimali ya gesi asilia inayochimbwa hapa nchini.