Ufaransa imefungua ofisi ndogo mpya za ubalozi na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) mkoani Dodoma.
Ufunguzi huo umefanyika katika eneo la Domiya Estate na kuhudhuriwa na wadau wa mashirika na viongozi mbalimbali wa serikali ya Tanzania pamoja na Ufaransa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Stargomena Tax amesema, kufunguliwa kwa ofisi hiyo ni mwendelezo wa juhudi za serikali katika kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali.
Ameongeza kuwa kutokana na shughuli nyingi za kiserikali kufanyika Dodoma, kuwepo kwa ofisi za ubalozi wa Ufaransa jijini Dodoma kutaongeza chachu ya huduma za kidiplomasia baina ya pande zote mbili.
Kwa upande wake balozi wa Ufaransa nchini Nabil Hajlaoui amesema, nchi hiyo inatambua jitihada za serikali ya Tanzania katika kukuza na kuimarisha makao makuu ya nchi, hivyo kuanzishwa kwa ofisi mpya kunaashiria dhamira ya Ufaransa ya kuimarisha uhusiano wake na Tanzania.