Ucheleweshaji wa upelelezi wamkera Rais

0
206

Rais John Magufuli amesema bado kuna ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa idara ya mahakama nchini, hali ambayo haimfurahishi.

Akihutubia jijini Dar es salaam katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini, Rais Magufuli amesema kuwa ukosefu huo wa maadili miongoni mwa watumishi wa idara ya mahakama umekua ukisababisha wananchi kukosa haki, kuwepo kwa idadi kubwa ya mahabusu zaidi ya wafungwa na kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi mbalimbali.

“Hii inadhihirisha kwamba tatizo la uchelewashaji kesi bado lipo, na hili Mheshimiwa Jaji Mkuu amelisema, jambo hili linawahusu zaidi wapelelezaji, mwakilishi wa IGP yupo na vyombo vingine vya TAKUKURU vipo hapa viharakishe suala la upepelezaji, linawanyima haki Wananchi,” amesema Rais Magufuli.

Amewataka watumishi wote wa idara ya mahakama nchini kuzingatia maadili ya taaluma zao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kushirikiana na vyombo vingine kuhakikisha idadi ya wafungwa magerezani pamoja na mahabusu inapungua.

“Wafungwa ni 13,000 na kitu mpaka leo, lakini mahabusu ni 17,632. Bado katika eneo hili haijafanyika kazi vizuri, na hili siyo suala la mahakama kwani ninyi majaji na mahakimu mnasubiri kuletewa,” amesema Rais Magufuli.

Kauli mbiu ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu ni Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.