Uchaguzi wa Ubunge Temeke kufanyika Januari 2019

0
1984

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Temeke mkoani Dar es salaam na kwenye kata 46 za Tanzania Bara.

Akitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo,  Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika Januari 19 mwaka 2019 na fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kuanzia Disemba 14 hadi 20  mwaka huu.

“Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe 20 Desemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 21 Desemba hadi tarehe 18 Januari mwaka 2019 na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 19 Januari mwaka 2019,” amesema Jaji Kaijage.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo.

Jaji Kaijage ameongeza kuwa uchaguzi huo mdogo katika nafasi ya udiwani utafanyika ndani ya halmashauri 28 zilizopo kwenye mikoa 14 ya Tanzania Bara.

Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Temeke mkoani Dar es salaam unafanyika kufuatia kujiuzulu uanachama wa Chama Wananchi (CUF) kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo Abdalla Mtolea.