Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka waandishi wa habari mitandaoni (Online na Bloggers) kuzingatia maadili na weledi wa kazi katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari wa mitandao, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt. Wilson Mahera amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari kufuata misingi na kanuni za uandishi katika kuripoti masuala ya uchaguzi.
Mahera amesema mitandao ina nguvu kubwa na ina wafuatiliaji wengi hivyo waandishi watumie fursa hiyo kutoa elimu ya mpiga kura na taarifa zinazohusu uchaguzi.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) anayeshughulikia leseni, Mhandisi Andrew Kisaka amesema vyombo vya habari vinatakiwa kutenda haki kwa vyama vyote, visiegemee upande wowote kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni za mamlaka hiyo.
Pia, amesema ni vema waandishi wakajiepusha na ushabiki wa wanasiasa badala yake waripoti uhalisia wa mambo yanayoendelea kwa weledi kuelekea uchaguzi.
Kadama Malunde ni miongoni mwa waandishi walioshiriki mkutano huo, ambapo ameishukuru tume ya uchaguzi kwa kuandaa mkutano huo kwa wanahabari wa mitandaoni kwani utaongeza ufanisi wa kuripoti habari za uchaguzi.