Wakandarasi wa ndani wametakiwa kutumia wataalamu wenye sifa katika kutekeleza shughuli zao, ili kukidhi vigezo hitajika na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akifungua mkutano wa tatu wa kikanda wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2023 ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa wadau wa ujenzi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Mhandisi Kasekenya amesema hatua hiyo pia itapunguza matumizi ya Wakandarasi wa nje hususani katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.
Amesisitiza kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa taasisi binafsi hususani katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Serikali kupitia taasisi kama Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wako katika hatua za mwisho za kukamilisha mkakati wa namna ya kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza majukumu yao,mfano tu ukikamilika mradi wa SGR ,kutakuwa na vipande vitakavyokuwa vikifanyiwa ukarabati na sekta binafsi badala ya TRC wenyewe”. Amesema Mhandisi Kasekenya
Akizungumza wakati wa mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB Mhandishi Joseph Nyamhanga ameishukuru Serikali kwa kupuguza matumizi ya force akaunti hasa katika ujenzi, hali iliyoamsha tena hari ya Wakandarasi wa ndani kufanya kazi.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Makanadarisi Mhandisi Rhoben Nkori ametoa wito kwa Wakandarasi wa ndani kuandika bei halisi ya miradi yao,wakati wa usajili wa miradi hiyo CRB, kwani baadhi yao wamekuwa wqkiandika gharama ndogo ya miradi tofauti na mikataba waliyoingia.