Zaidi ya watumishi 850 wa Idara ya mahakama nchini , wengi wao wakiwa ni mahakimu wameajiriwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015.
Lengo la kuajiri watumishi hao ni kuharakisha mashauri mbalimbali pamoja na kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa katika magereza hapa nchini.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Rais John Magufuli wakati akifunga mkutano wa 11 wa bunge, halfa iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali pamoja na viongozi wastaafu.
Amesema jambo jingine lililofanywa na serikali ili kuhakikisha msongamano wa mahabusu na wafungwa unapungua ni kuteua majaji 17 wa mahakama ya Rufani na wengine 52 wa Mahakama Kuu na kujenga mahakama kuu mbili na kukarabati nyingine nne katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, katika kipindi cha miaka mitano zaidi ya wafungwa elfu 42 wa makosa mbalimbali wamesamehewa na mahabusu wengine wengi wamefutiwa mashtaka.
Ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kufanya kazi nzuri katika kuhakikisha msongamano wa mahabusu na wafungwa unapungua.