Tukio la tembo kuua Watu watatu lachunguzwa

0
172

Jeshi la Polisi mkoani Kagera linaendelea kuchunguza tukio la watu watatu ambao ni mume, mke na mtoto kufariki dunia na mwingine mmoja kujeruhiwa baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na tembo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kagera, – Revocatus Malimi amewataja walioafariki dunia kuwa ni Fred Muhire, Aneth Fred na Angel Fred.

Amesema kuwa tukio hilo limetokea katika kijiji cha Nshabaiguru wilayani Karagwe wakati Aneth akienda kisimani kuchota maji huku akiwa amembeba mtoto wake mgongoni.

Amesema kuwa mama huyo akiwa njiani alikutana na kijana mkazi wa kijiji hicho akikimbia na kumwambia anafukuzwa na tembo, na kumtaka kukimbia, lakini hata hivyo hakufanikiwa maana tembo alikuwa amekwishamkaribia na kuanza kumshambulia pamoja na mwanae na kuwajeruhi.

Amesema mume wa mama huyo akiwa katika shughuli zake, alipata taarifa kuwa familia yake imevamiwa na tembo ndipo alikimbia kwenda kutoa msaada, lakini naye akakutana na tembo na kushambuliwa, na kufariki dunia papo hapo.

“Majeruhi hao walipelekwa katika hospitali ya Nyakahanga kwa matibabu, lakini wawili walipoteza maisha usiku huo, na kubakia majeruhi mmoja Juma Rashida ambaye anafanya kazi ya kuchunga ng’ombe na hali yake inaendelea vizuri,” amesema. Kamanda Malimi.