TUCTA yaomba kuongezwa kima cha chini cha mshahara

0
200

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakzi Tanzania (TUCTA), limeiomba Serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara na kufikia shilingi Laki Tisa na elfu Sabini kwa mwezi.

Ombi hilo limetolewa mkoani Mwanza na Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Said Wamba wakati wa kilele cha sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zinazofanyika kitaifa mkoani humo.

Wamba amesema Watumishi wa umma wamefanya kazi bila kuongezewa mshahara kwa kipindi cha miaka sita sasa, hivyo wanastahili nyongeza hiyo ya mshahara ili waweze kumudu hali ya maisha.

Mbali na ongezeko la mishahara, TUCTA pia imeitaka Serikali kuhakikisha inasimamia maslahi ya Watumishi katika sekta binafsi, ambayo imekaa bila kuongezewa mshahara kwa zaidi ya miaka kumi.

Aidha TUCTA imeitaka Serikali kusimamia utoaji wa huduma ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwani ilivyo sasa Watumishi wengi wamekuwa wakipata usumbufu wa kupata huduma licha ya kukatwa na Waajiri wao.