Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu kwa Wakulima nchini inayohusu aina za Wakulima wanaotambuliwa kisheria na misamaha ya kodi inayoigusa sekta ya kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya, Afisa wa TRA Nicodemus Massawe amesema misamaha ya kodi iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 kwa sekta ya kilimo inahusisha ununuzi wa matrekta kutoka nje ya nchi, vifaa vya ujenzi wa greenhouse [nyumba za kupandia mazao], mbolea na pembejeo zingine zinazohusiana na kilimo.
Amewakumbusha wakulima kuwa sio wakulima wote wanaopata msamaha wa kodi, kwani sheria inatambua aina mbili za wakulima na kuwataja wakulima hao kuwa ni mkulima wa kilimo cha biashara na yule wa kilimo cha familia au kujikimu.
Massawe
amefafanua kuwa mkulima wa kibiashara atatakiwa kulipa mapato na msamaha huo hautomhusu huku yule wa kilimo cha kujikimu au kifamilia ndiye atakayepata msamaha wa kodi katika kilimo chake.
Aidha, amesisitiza kuwa sheria hiyo ya kodi inawajumuisha hadi Wafugaji na sio Wakulima peke yao.