Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuweka alama zinazoonekana kuzunguka eneo la mradi wa Kuchakata na kusindika Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Likong’o wilayani Lindi, Mkoa wa Lindi.
Dkt.Kalemani ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo hilo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi na wawekezaji wa mradi huo, kampuni ya Equinor na Shell.
“ Eneo hili tumeligharamia hivyo ni muhimu likawekwa alama zinazoonekana badala ya kuweka bango pekee ili eneo hili liweze kutambulika na wananchi wasije kulivamia au kutumika vibaya, hivyo tuna wajibu wa kulinda eneo hili na kuonesha kuwa kuna kazi inakuja.” Amesema Dkt.Kalemani
Aidha, Dkt. Kalemani ametoa agizo kwa TPDC kuwa ndani ya siku Tano wawe wamekamilisha taratibu za upatikanaji wa mkandarasi kutoka mkoani Lindi atakayeweka alama hizo za mipaka na mkandarasi huyo aanze kazi mara moja.
Aidha, ametoa agizo kwa TPDC kuhakikisha kuwa, eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2,071 linasafishwa na kuwaasa wananchi kutovamia eneo hilo kwani limeshatwaliwa na Serikali baada ya wananchi hao kulipwa fidia.
Dkt. Kalemani amewaeleza wadau hao kuwa, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 5.72 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa eneo hilo kazi ambayo ilikamilika mwaka jana.
Ameongeza kuwa, mwezi Mei mwaka huu majadiliano yameanza na wawekezaji kuhusu utekelezaji wa mradi huo na yanatarajiwa kufikia mwisho mwezi Oktoba mwaka huu.