TPDC kuuza gesi asilia nje ya nchi

0
135

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limegundua futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia, ambapo mchakato wa uvunaji utakapokamilika itaimarisha soko la ndani na kuuza nje.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Dkt. Mataragio amesema kiasi kikubwa cha gesi hiyo, kimegundulika baharini.

“Kiasi kikubwa cha gesi kipo baharini, tunatarajia kukivuna, kwa sasa tunaendelea na mtambo wa LNG ambao utachakata gesi hiyo,” amesema Dkt. Mataragio

Amesema mchakato wa kuvuna gesi hiyo utakapokamilika, itasafirishwa kwenda kwenye masoko ya nje na kiasi kitakachobaki kitatumika kwa ajili ya soko la ndani.

TPDC inaendelea kujenga vituo vingine zaidi ili kusogeza huduma kwa wananchi, mchakato utakaokamilika mwaka 2023.

“Tutakuwa na vituo zaidi, mteja atakuwa anaenda kwenye vituo vyetu ili kuweza kuweka gesi anayoihitaji.” amesema Dkt. Mataragio