Wafanyabiashara wakiwemo wa hoteli na viwanda katika eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam wameipongeza Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuanza mchakato wa kuwaunganishia miundombinu ya mabomba ya kuunganishiwa gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea mitambo na kupikia.
Wakizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam Wafanyabiashara hao wamesema, baada ya kutathmini gharama za uendeshaji kwa kutumia nishati ya sasa na gesi asilia wanatarajia kupunguza zaidi ya asilimia 40 ya gharama zinazotumika sasa.
Meneja wa Operesheni wa hoteli ya White Sands Ali Hilika amesema baada ya kufanya tathmini, wameamua kubadili mfumo wa kutumia nishati ya sasa na kuomba kuunganishiwa gesi asilia kwa kuwa ni nafuu na salama zaidi.
Naye Mhandisi Mkuu wa hoteli ya Lamada, Prabhu Murugesan ameshauri kuongezeka kwa kasi ya ufungaji wa miundombinu hiyo ya mabomba ya kuunganishiwa gesi asilia ili waanze haraka kutumia nishati hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC Marie Msellemu amesema wameunganisha miundombinu katika hoteli sita na viwanda viwili na kuwataka Wananchi kuomba kuunganishiwa nishati hiyo ambayo ni nafuu na salama zaidi kutumia.