TPA yaagizwa kuimarisha usimamizi wa Flow Meters

0
158

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inaendelea kuimarisha usimamizi wa mitambo ya mita za upimaji wa mafuta (Flow Meters) ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kukagua mitambo ya mita za upimaji wa mafuta ya Kigamboni na Kurasini Oil Jety (KOJ) kwenye bandari ya Dar es salaam. 

Akitoa agizo hilo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, Serikali inataka kuona makusanyo yote ya mapato kutoka katika bandari zote nchini yanayokusanywa na TPA yanaingia katika mfuko mkuu wa Serikali na haitakubali kubaki na mtu anayejihusisha na upotevu wa mapato hayo.

Hata hivyo Waziri Mkuu ameeleza kuridhishwa na utekelezwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali ambayo amewahi kuyatoa kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2016 alipofanya ziara katika eneo la mitambo hiyo ya mita za upimaji wa mafuta ya Kigamboni na KOJ.

Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania kuimarisha usimamizi wa mitambo hiyo na kuanzisha idara maalum ya kuzisimamia katika bandari zote hapa nchini.