Wakurugenzi wa halmashauri zenye masoko ya samaki ya Kimataifa wametakiwa kuacha kupanga tozo za mazao ya uvuvi bila kuwasiliana na wizara ya Mifugo na Uvuvi, lengo likiwa ni kuondoa kero za tozo kwa Wananchi wanaofanya biashara katika maeneo hayo.
Agizo hilo limetolewa wilayani Chato mkoani Geita na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki mara baada ya kutembelea mnada wa mifugo uliopo katika kijiji cha Buzirayombo na soko la samaki la kimataifa lililopo kwenye kijiji cha Kasenda.
Amesema wizara haitaki kusikia kero za Wafanyabiashara kuhusu tozo zisizo rafiki katika masoko hayo pamoja na masoko mengine likiwemo lile la samaki la kimataifa la Kata ya Kirumba lililopo wilayani Ilemela jijini Mwanza.
“Kuhusu tozo niseme tu kwa Wakurugenzi walio na masoko haya ya Kimataifa kwa maana ya soko la Kirumba na Kasenda, sisi wizara hatutaki kusikia kelele katika haya masoko, mnapopanga tozo zenu hakikisheni kwa masoko haya mawili tuwasiliane ili tupange tozo za kwenu na kwetu ambazo zitakuwa rafiki”,amesema Waziri Ndaki.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt Medard Kalemani amemuomba Waziri Ndaki kupitia vikundi vya wavuvi vilivyosajiliwa, wizara ione namna ya kuwasaidia wavuvi mikopo yenye riba nafuu pamoja na kuwanunulia nyavu ili kuacha kujihusha na uvuvi usiofuata taratibu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amekagua pia ujenzi wa machinjio ya kisasa yanayojengwa katika eneo la mnada wa mifugo katika kijiji cha Buzirayombo wilayani Chato.