Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa msaada wa dawa za kutibu binadamu kwa Jeshi la Magereza mkoani Mara ambazo zitatumika kwa ajili ya kuwatibu wafungwa na mahabausu waliopo ndani ya Mkoa huo.
Dawa hizo zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 23 zinatokana na msako ambao umekuwa ukifanywa na mamlaka hiyo katika maduka mbalimbali ya dawa, na zitasambazwa kwenye zahanati zilizo chini ya jeshi la magereza
Akikabidhi msaada huo meneja wa kanda hiyo, Sophia Mziray amesema ofisi yake imekuwa na utaratibu wa kutoa dawa kwa taasisi mbalimbali ikiwemo magereza na itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za Serikali ikiwemo magereza ili kuhakikisha kuwa binadamu wanapata tiba bora na ya viwango.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Juma Mfanga amesema upo upungufu wa dawa katika hospitali za magereza hivyo msaada huo utakwenda kupunguza tatizo hilo, huku akiwataka wahusika kutumia msaada huo kwa lengo lililokusudiwa.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Hospitius Mendi ameiomba taasisi hiyo kuendelea kutoa msaada wa aina hiyo kwani mahitaji ya dawa ni makubwa