TICAD 7 kuanza Agosti 28

0
230

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi yupo jijini Yokohama, -Japan kwa ajili ya kushiriki mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) utakaofanyika kuanzia Agosti 28 hadi 30 mwaka huu.

Mkutano huo utatanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Makatibu Wakuu na Mabalozi, ukifuatiwa na kikao cha Mawaziri na utahitimiswa na mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika utatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotekelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Wakati wa mkutano huo, nchi zote zimepatiwa nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na vivutio vya utalii wa nchi husika, ambapo Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB) itatumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo akimwakilisha Rais John Magufuli.

Kauli mbiu ya mkutano huo wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) ni kuendeleza maendeleo ya Afrika kupitia watu, teknolojia na uvumbuzi.

Mwaka 1993 Japan ilianzisha jukwaa la majadiliano kati yake na nchi za Afrika, kwa lengo la kujadili maendeleo na nchi hizo.