TET kufanya mapitio ya sita ya mitaala

0
116

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imesema tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, imefanya mapitio makubwa sita ya mitaala ya elimu lengo likiwa ni kuwajengea wahitimu ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kutumia vema fursa zinazopatikana nchini, husani kwa kujiajiri, kuajiriwa na kumudu maisha yao ya kila siku pale wanapohitimu mafunzo.

Kati ya mapitio hayo, matano tayari yalishafanyika mpaka kufikia mwaka 2014, na sasa kazi ya kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya pitio la sita inaendelea.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Aneth Komba amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam kuhusu uetekeleza wa shughuli za Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na mwelekeo wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Aidha ameeleza kuwa katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilitoa Fedha jumla ya Shilingi Bilioni 1.4  ambazo zimetumika kukusanya maoni ya wadau, kuchakata taarifa na kuandaa rasimu za mitaala ya ngazi zinazopendekezwa

Akizungumzia Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, Dkt. Komba amesema TET imejipanga kuwashirikisha wadau kuhusu rasimu za mitaala zilizopendekezwa, na kuendelea na hatua ya kuandaa vifaa vingine vya utekelezaji wa mitaala ikiwemo mihtasari pamoja na kutoa mafunzo ya walimu na wasimamizi wengine wa utekelezaji wa mitaala.