Tehama kitaifa na kimataifa

0
245

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakusudia kuwa kitovu cha fursa katika sekta ya TEHAMA kitaifa na kimataifa.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua kikao kazi cha uchambuzi wa fursa za kiuchumi za sekta ya mawasiliano kitaifa na kimataifa.
 
Ameongeza kuwa serikali imelenga kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA ili waweze kutumia vema fursa zinazokuwa zinajitokeza ndani na nje ya Tanzania.
 
“Serikali imeweza kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo watu pamoja na wadau ili kuhakikisha tunakuza sekta hii ya mawasiliano, kama mnavyofahamu lazima tutekeleze mpango wa maendeleo kwa kuangalia yaliyomo ndani ya nchi yetu pamoja na mambo yanayoweza kuhamasisha,”amesema Dkt.Yonazi
 
Amesema wizara hiyo ina jukumu la kuchambua na kuangalia ni nchi zipi Tanzania inaweza kushirikiana nazo, lakini pia kuangazia suala la ujenzi wa minara na kuongeza uwezo wa kutumia simu janja pamoja na usalama wa mtandao.

Lengo la kikao kazi hicho cha uchambuzi wa fursa za kiuchumi za sekta ya mawasiliano kitaifa na kimataifa ni kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kukuza uchumi kupitia TEHAMA pamoja na fursa zingine zilizo kitaifa na kimataifa.