TEA yapiga tafu ujenzi wa mabweni

0
189

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amefungua rasmi mabweni mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari ya Kainam wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.

Akifungua mabweni hayo, Waziri Bashungwa ameipongeza TEA kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni hayo.

Naye Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Kainam, Atnasi Massay amesema mradi huo umesaidia wanafunzi kufanya vizuri, kwani umewaepusha na vishawishi kwa kuishi katika mazingira yenye utulivu.

“Kupitia mradi huu wa mabweni watoto wetu wamepata fursa ya kusoma na kupata utulivu, na taaluma ya shule yetu imekuwa kwa maana sasa ni ya kwanza katika halmshauri ya Mji wa Mbulu kitaaluma kwa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne na cha pili mwaka 2020 na 2021.” amesema mwalimu Massay

TEA kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa imetumia shilingi bilioni 1.39 kwenye miradi mbalimbali mkoani Manyara katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020.