TCRA yamshushia rungu Polepole

0
123

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kali na kukisimamisha kwa muda kipindi cha Shule ya Uongozi kinachoendeshwa na Humphrey Polepole ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa kupitia televisheni ya mtandaoni ya Humphrey Polepole Online TV, mpaka hapo televisioni hiyo itakapofuata vigezo na masharti yaliyowekwa na mamlaka hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya televisheni hiyo kutangaza maudhui yanayodaiwa kupotosha umma likiwemo suala la ugonjwa wa UVIKO – 19, matumizi ya fedha za Serikali, deni la Taifa pamoja na suala la Wafanyabiashara wadogo.Akisoma hukumu hiyo mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Maudhui ya TCRA Ndalahwa Gunze amesema, kamati hiyo imejiridhisha kuwa Television hiyo haina waandishi wenye taaluma ya uandishi wa habari pamoja na utangazaji.

Kwa upande wake Polepole ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema, amepokea uamuzi kamati hiyo ya Maudhui ya TCRA na atakapokuwa tayari atazungumza suala hilo.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, rufaa juu ya hukumu hiyo ipo wazi kwa mmiliki wa televisioni hiyo.