Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya watu wote wanaotoa taarifa kuhusu homa ya corona na kudai kuwa ni sahihi, kuacha mara moja vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesema kuanzia sasa taarifa kuhusu virusi vya corona hapa nchini zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ikilazimika zitatolewa na Waziri Mkuu na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha mkanganyiko.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa onyo hilo wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa mikoa yote nchini, mkutano uliofanyika kwa njia video akiwa ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.
Kufuatia kuwepo kwa watu hao ambao wamekua wakitoa taarifa kuhusu corona kinyume na utaratibu, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ifuatilie watu wote wanaofanya upotoshaji kwa kupitia mitandao ya kijamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Watu wote wanaopotosha umma na kuleta taharuki kuhusu ugonjwa wa corona badala ya kuelimisha namna ya kujikinga, wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Amesema licha ya hali ya maambukizi ya corona nchini kutokua ya kutisha, viongozi wa mikoa yote nchini, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa mikoa yote nchini hawana budi kupeana taratibu za namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Wakuu wa mikoa kila mmoja ahakikishe eneo lake linakuwa salama na endapo kutakuwa na mgonjwa tumieni zahanati ambazo bado hazijaanza kutumika kwa ajili ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa corona,” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Amewataka wakuu hao wa mikoa waimarishe utoaji wa elimu kwa umma na ikiwezekana watumie magari ya matangazo ili wananchi waelewe athari za homa ya corona na namna ya kujikinga pamoja na kuwaondolea hofu ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanawafuatilia na kuwachukulia hatua, wafanyabiashara wote watakaobainika kuongeza bei kwa bidhaa ambazo zinatumika katika udhibiti wa maambukizi ya homa ya corona.
