Ikiwa jukwaa la majadiliano ya masuala ya kisiasa katika wilaya mbalimbali hapa nchini litatumika ipasavyo, ufanisi katika masuala ya kidemokrasia utaongezeka.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarouk Seif Salim wakati wa uzinduzi wa jukwaa la majadiliano la vyama vya siasa wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja.
Mbarouk amesema jukwaa hilo lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) linawakutanisha viongozi na wajumbe wa vyama vya siasa kujadili changamoto zinazowakabili ili kufikia maendeleo ya kidemokrasia.
Afisa Mradi wa Majadiliano TCD, Likele Shungu amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya siasa ili waweze kutekeleza wajibu wao kidemokrasia zaidi.
Walioshiriki mkutano huo ni wajumbe kutoka vyama vya CCM, CUF, CHADEMA, NCCR MAGEUZI na ACT Wazalendo na mada zilizowasilishwa ni kuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa pamoja na uvumilivu wa kisiasa.