TCAA yaonyesha nia ya kuifuta Fastjet

0
1526

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA) imetoa notisi ya siku 28 ya nia ya kulifuta Shirika la Ndege la Fastjet ikilitaka kuhakikisha linaandaa mpango kazi utakaoonyesha ni kwa namna gani litajiendesha kwa ufanisi.

Notisi hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, -Hamza Johari na kuongeza kuwa endapo shirika hilo litashindwa kufanya hivyo litafutiwa leseni ya uendeshaji biashara ya usafiri wa anga.

Johari amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa wameamua kutoa notisi hiyo kufuatia mwenendo usioridhisha wa Fastjet katika utoaji wa huduma zake.

“Fastjet imepoteza sifa za kutoa huduma, na hivyo TCAA inakusudia kufuta cheti cha biashara cha shirika hilo” ,amesisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo wa TCAA.

Katika notisi hiyo ya siku 28 inayofikia kikomo Januari 14 mwaka 2019, shirika hilo limeelekezwa kuandaa mpango kazi, mpango wa fedha na mpango wa biashara pamoja na kuwa na meneja uwajibikaji mwenye weledi kuhusu usafiri wa anga.

Notisi hiyo pia inaitaka fastjet kusitisha mauzo ya tiketi kwa wateja wapya, kuwarejeshea fedha wale wote ambao wameshalipia tiketi zao au kuwaombea safari katika mashirika mengine pamoja na kuwafidia wale wote waliopata madhara kwa mujibu wa sheria.

Fastjet pia imetakiwa ilipe madeni yote inayodaiwa.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa TCAA amewataka
wadau wengine ambao watakuwa na madeni mbalimbali kwa shirika hilo la Fastjet wapeleke taarifa zao katika Mamlaka hiyo ya Usafiri wa Anga.