TBC yapiga kambi kuwanoa maafisa Habari

0
232

Katika juhudi za kuhabarisha umma na kuendana na Kasi ya teknolojia, Shirikisha la Utangazaji Tanzania (TBC) limeandaa mkutano wa 104 wa washitiri wa vipindi vya elimu kwa umma ambapo maafisa habari wa taasisi na mashirika mbalimbali wamehudhuria kwenye mafunzo hayo.

Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema pamoja na kutoa mada mbalimbali zitakazowasaidia maafisa hao wa habari lakini pia TBC imejipanga kuboresha njia za uwasilishaji wa habari, matukio na vipindi kwa jamii kupitia mitandao yake ya kijamii ili kuendana na teknolojia ya sasa ya upashanaji habari.

“Sasa hivi TBC tunataka kuhakikisha tunaboresha zaidi mitandao yetu ya kijamii kuhakikisha tunaifikia jamii yote ili kwenda na kasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa haraka zaidi maana jamii kubwa inahitaji kuhabarishwa kwa haraka na umakini,” ameeleza Dkt. Rioba.

Baadhi ya maafisa habari kutoka taasisi na mashirika ya umma akiwemo Magret Harrison kutoka wizara ya ardhi, amesema wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi za ardhi na wangependa kujua utatuzi wa changamoto hizo kwa kupata taarifa sahihi na kwa haraka zaidi hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Dennis Buyekwa amesema ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ina wajibu wa kuhakikisha taarifa zote zinazohusu kesi na hukumu mbalimbali zinazotolewa kwa serikali katika kesi za ndani na nje ya nchi zinawafikia wananchi.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu unaofanyika mkoani Morogoro ni “Dhima ya mawasiliano kwenye kuhabarisha na kushirikisha wananchi katika maendeleo ya uchumi wa kati yenye sura ya utu.”