TBC yamwagiwa sifa kwa mapinduzi iliyoyafanya

0
288

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeeleza kuridhishwa na mapinduzi ya
upashanaji habari yaliyofanywa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kulitaka shirika hilo kuendelea kuboresha matangazo yake.

Wajumbe wa kamati hiyo wamesema hayo mara baada ya kukagua jengo la studio za TBC na kutembelea ofisi nyingine kujionea utendaji kazi unavyofanyika.

Baadhi ya mambo ambayo yamewafurahisha Wajumbe hao ni ujenzi wa studio za kisasa, ambazo zitarahisisha urushaji wa matangazo kuendana na kasi ya karne ya 21 na uboreshaji wa mifumo mingine ya urushaji matangazo, mathalani ukarabati wa studio ya Aridhio.

Uwepo wa watangazaji watanashati, wenye uwezo na weledi pamoja na maadili ya tasnia ya habari, ni sehemu nyingine ambayo imewavutia Wajumbe wa kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii.

Sifa nyingine zimetokana na TBC kuzingatia usawa wa kijinsia katika nyadhifa za uongozi katika nafasi za juu za uongozi.

Hata hivyo kamati hiyo imeitaka TBC kuendeleza ubunifu, kuzingatia weledi na kutoa habari kwa kuzingatia mizania ili wananchi waendelee kuiamini na wapate habari na taarifa zenye ubora.