TBC na Voice of Nigeria zasaini mkataba wa ushirikiano

0
262

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Voice of Nigeria (VON) zimesaini mkataba wa makubaliano (Memorandum of Understanding) ya kushirikiana, kukuza na kubadili mtazamo wa habari za Kiafrika kwa ulimwengu.

Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha alipotembelea taasisi hiyo na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa VON, Osita Okechukwu jijini Abuja, Nigeria.

Okechukwu amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu kwa ajili ya kukuza harakati za Afrika (Pan-Africanism) kama zilivyoasisiwa na viongozi wa Afrika kama Dkt. Nnamdi Azikiwe, Abubakar Tafawa Balewa na Julius Nyerere.

Kwa upande wake Dkt. Rioba amesema kuwa VON inatoa jukwaa la kuuzungumza ukweli wa Afrika kwa Afrika na dunia kwa ujumla.

Ameongeza kuwa ziara yake inalenga kuanzisha uhusiano, kukuza lugha ya Kiswahili na kukuza ubadilishanaji wa programu kwa manufaa ya pande zote mbili.

Baada ya kusaini makubaliano hayo ujumbe huo ulipata nafasi ya kutembelea Mamlaka ya Televisheni Nigeria na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mallam Yakubu Ibn Mohammed.