Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF) kupitia mradi wa Cookfund yanalenga kushirikiana kuelemisha jamii kuhusu matumizi ya nishati mbadala ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo utanzaji wa mazingira na kuondokana na madhara yatokanayo na nishati isiyo safi.
Mazungumzo ya kulenga ushirikiano huo yamefanyika katika ofisi za TBC Mikocheni, Dar es Salaam wakati viongozi wa UNCDF wakiongozwa na Mkuu wa UNCDF Tanzania, Peter Malika walipotembelea TBC na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha.
Malika amesema kupitia mradi wao wanalenga kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kuendana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na mpango wa Serikali kuelekea matumizi ya nishati mbadala kufikia mwaka 2024 kwa taasisi zenye chini ya watu 100 na mwaka 2025 kwa taasisi zenye watu chini ya watu 200.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema TBC imekuwa mstari wa mbele kusimamia, kutunza na kuelemisha jamii kuhusu utanzaji wa mazingira kupitia vipindi mbalimbali vinavyorushwa na TBC.