TBC na UCSAF kuzindua studio za kisasa za redio Dodoma

0
164

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), limeendelea kutekeleza Miradi ya Upanuzi wa Usikivu wa TBC ambao una lengo la kupeleka huduma ya mawasiliano na habari kwa umma kwa njia ya redio.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa ujenzi wa mitambo ya redio ya masafa ya FM pamoja na ukarabati wa studio na ufungaji wa mitambo ya redio jamii eneo la Uhindini, jijini Dodoma yamefanyika kwa kushirikiana UCSAF.

Dkt. Rioba amesema Oktoba 27, 2018, TBC na UCSAF zilisaini mkataba wenye thamani ya shilingi bilioni 1.014 kwa ajili ya mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa umeongeza usikivu wa matangazo ya TBC katika maeneo mbalimbali nchini.

“Leo tumewaita hapa (wanahabari) kwa ajili ya kuwaeleza kuhusiana na uzinduzi wa redio yetu ya jamii katika makao makuu ya nchini, Dodoma siku ya Jumatatu, ambapo mawaziri wetu wawili watashiriki katika uzinduzi huo,” amasema Dkt. Rioba.

“Mradi huu[o] ni sehemu ya miradi iliyotekelezwa kwa ushirikiano kati ya TBC na UCSAF. Miradi ya aina hii ya ujenzi wa studio za redio jamii ni sehemu ya miradi ya kimkakati kwa ajili ya kufikia mawasiliano na habari kwa wananchi,” amesisitiza Dkt. Rioba.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema wataendelea kushirikiana na TBC katika kuboresha usikivu wa redio zake kwa lengo la kuwapa fursa wananchi ya kusikiliza vipindi na habari mbalimbali.