TBC kushirikiana na chuo cha Mweka

0
96

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na Chuo cha Usimamizi na Uhifadhi wa Wanyamapori (MWEKA) kilichopo mkoani Kilimanjaro, wamekubaliana kutangaza moja kwa moja shughuli ambazo Chuo hicho kinazifanya wakati wanafunzi wanapokuwa katika mafunzo ya vitendo katika hifadhi mbalimbali nchini kupitia chaneli ya Tanzania Safari.

Kauli hiyo imetolewa wilayani Moshi na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt Ayoub Rioba alipotembelea Chuo hicho na kuongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kukuza utalii nchini pamoja na kuwawezesha Watanzania wengi kufahamu shughuli zinazofanywa na chuo hicho.

Dkt Rioba amesema kuwa, TBC watakuwa wanarusha mafunzo yote ya vitendo ambayo wanafunzi wanafanya wawapo katika Hifadhi na mbuga mbalimbali nchini, huku wakiwatumia Wataalamu wa chuo hicho kuelezea tabia za Wanyama katika Makala zitakazorushwa katika chaneli ya Tanzania Safari.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha MWEKA, Profesa Jafari Kideghesho amesema kuwa, ushirikiano huo utasaidia pia kutangaza utalii pamoja na kuhamasisha Watanzania kujiunga na chuo hicho.