TBC iwe sauti ya wanyonge

0
119

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew ameliagiza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuwa sauti ya watu wasioweza kusema.

Mathew ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TBC leo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema wafanyakazi wa TBC wanapaswa
kuendelea kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kuiwasilisha vyema kaulimbiu ya Shirika ya Ukweli na Uhakika ili kuchochea maendeleo ya Taifa.

Waziri Kundo amesema Serikali itahakikisha kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linajitosheleza kifedha na rasilimali watu, huku ikiendelea kuboresha usikivu kwa maeneo ya mijini na vijijini ili kuwafikia wananchi katika maeneo yote.

Kwa upande mwingine Kundo amesisitiza TBC kuendelea kutoa maudhui yatakayotunza amani na utamaduni wa taifa la Tanzania.

Aidha, amesema TBC inapaswa kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi, ikiwafikishia taarifa sahihi kwa wakati.