TBA yaagizwa kutekeleza miradi yenye ubora

0
75

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha miradi ya ujenzi wanayotekeleza inazingatia ubora, tija, gharama nafuu pamoja na ujenzi wa kisasa unaoendana na wakati.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo mkoani Dodoma, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa nyumba 3,500 za watumishi wa umma, zinazojengwa na TBA katika eneo la Nzuguni.

Amesema ni vema TBA ikafanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji, kuongeza ubunifu na kujenga misingi mizuri ya kujiendesha kibiashara, ili kuweza kupata mapato zaidi na kujiendesha pasipo kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Aidha Makamu wa Rais ameitaka wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuharakisha mchakato wa marekebisho ya kanuni ya uanzishwaji wa Wakala wa Nyumba Tanzania, ili taasisi hiyo iweze kukamilisha taratibu zote za kuingia ubia na wawekezaji hali itakayopunguza utegemezi wa ruzuku ya serikali pekee katika kutekeleza miradi mikubwa.